Updates

TAHAFE Kutoa Tamko la Hijja

na mwandishi wetu

Mzozo huu wa Hijja umekuja mara baaada ya kuibuka kwa taarifa kupitia vyombo mbali mbali vya habari juu ya taasisi zinazo jishughulisha na masuala ya kusafirisha mahujaji kudaiwa takribani Shilingi Milioni 160 za Hijja ya mwaka jana na Serikali ya Saudi Arabia.

Shirikisho la Mahujaji hapa nchini (TAHAFE) limesema kuwa ndani ya wiki moja ijayo litatoa tamko juu ya sakata la HijJa ili kuondoa taharuki iliyopo. Katika mazugumzo kwa kupitia simu, Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Sheikh Abdallah Khalid aliahidi kutoa tamko hilo kufuatia habari iliyochapwa toleo la wiki iliyopita la gazeti hili kuhusu lawama zinazoelekezwa kwenye shirikisho hilo juu ya Hijja ya mwaka huu. “Tutawaiteni vyombo vya vyote vya habari ili tuwape taarifa rasmi Juu ya suala la Hijja. Fanyeni subira,” alisema Katibu huyo, Sheikh Khalid. Katika toleo lililopita gazeti hili lilimnukuu kiongozi mmoja wa taasisi inayojishughulisha na masuala ya usafirishaji wa mahujaji ambaye alisema kuwa watu wengi wako katika hali hiyo ya hofu kwa kuwa TAHAFE bado haijatoa tamko rasmi kuhusu kadhia hiyo. “Idadi ya watu huenda ikapungua mwaka huu kwani hadi sasa watu bado wana wasiwasi kutokana na kutotolewa kwa tamko rasmi kutoka Shirikisho la Mahujaji hapa nchini (TAHAFE) juu ya kadhia iliyotokea,” alisema kiongozi huyo. Kauli ya Wakfu na mali za amana Hata hivyo, wakati hali ikiwa hivyo huku Bara, gazeti la Imaan liliamua kufuatilialeo ya maandalizi ya ibada hiyo kwa upande wa Zanzibar ambapo Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali za Amana Zanzibar Sheikh Abdallah Twalib ambapo pia taasisi hiyo inashugulikia masuala ya Hija Tanzania bara na visiwani amesema kuwa Watanzania wajiandae na hakuna shaka yoyote juu ya uwepo wa ibada ya Hijja. “Hijja ipo hivyo Watanzania wajiandae kwani deni limekwishalipwa kwa kiasi kikubwa na kiasi kilichobaki hakiwezi kutuzuia kwenda Hijja,” alisema Sheikh Twalib. Sheikh Twalib aliongeza kuwa kwa sasa Tanzania tayari imeshaingia mkataba na Serikali ya Saudi Arabia na wamepewa idadi ya Mahujaji 2,700 mwaka huu. Mzozo huu wa Hijja umekuja mara baaada ya kuibuka kwa taarifa kupitia vyombo mbali mbali vya habari juu ya taasisi zinazojishughulisha na masuala ya kusafirisha mahujaji kudaiwa takribani Shilingi Milioni 160 za Hijja ya mwaka jana na Serikali ya Saudi Arabia. Fedha ambazo zilisemekana kudaiwa ni zile za mahema, pamoja na huduma wanazozipata Mahujaji wanapokuwepo kwenye ibada hiyo ya Hija, na muda wa mwisho ulitolewa kulipwa kwa deni hilo ilikuwa Februari 25 mwaka huu. Hali ya Zanzibar Kwa upande wa Zanzibar, Sheikh Khamisi Yussuf ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Taasisi za Hija Visiwani humo (UTAHIZA) amesema kuwa safari ya Hijja ipo kwa pande zote mbili za Muungano kwani suala la deni limeshughulikiwa vema. “Mzozo ule umepatiwa suluhu nzuri kwani ndugu zetu Watanzania bara wamejitahidi sana kulipa deni na hivyo ile hofu ya Tanzania kufungiwa haipo tena,” alisema Sheikh Yussuf, akiwamwagia sifa kemkem Tahafe. Sheikh Yussuf pia aliongeza kuwa wao kama Wazanzibar hawana ugomvi na taasisi za Hijja Tanzania bara kama inavyoelezwa na baadhi ya watu. “Sisi hatuna nia mbaya na taasisi za Hijja za Tanzania bara, lengo letu la kutoa habari ile lilikuwa jema, kwani tulitaka wenzetu wawahishe kulipa deni ili tusifungiwe,” alisema Sheikh Yussuf. Kuhusu safari za Hijja kwa upande wa Zanzibar, Sheikh Yussuf amesema kuwa matayarisho yanaendelea vizuri. “Matayarisho yanaendelea vema na tayari tumeshapeleka majina ya wahusika wa Hija huko Saudi Arabia ikiwemo kutafuta usafiri,” alisema Sheikh Yussuf. Hata hivyo Sheikh Yussuf amesema kuwa mahudhurio yanatarajiwa kuwa hafifu kutokana na mdororo wa uchumi uliopo nchini. “Tanzania kwa ujumla bara na visiwani tumepewa nafasi 2,700 ya Mahujaji na serikali ya Saudi Arabia ila hata hivyo huenda idadi hiyo isifikiwe kwani hali ya kiuchumi kwa sasa imedorora,” alisema Sheikh Yussuf. Kwa ujumla wake Tanzania hupewa nafasi 25,000-30,000 za Mahujaji kutokana na idadi ya wakazi wake, hata hivyo idadi hiyo haifikiwi kwa sababu za kiuchumi na muamko hafifu wa watu kuhusu ibada ya Hijja. Hii ni changamoto kwa Masheikh kuelimisha na kuhamasisha umma wa Kiislamu kutekeleza Hijja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*