Updates

Watanzania Waonesha Matumaini Kwa Taasisi ya Kikwete

Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete akiongea katika uzinduzi wa bodi ya wadhamini ya JMKF.

NA ABDULKARIM MSENGAKAMBA.

Baadhi ya Watanzania wameonesha kuwa na matumaini makubwa kwa taasisi mpya ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete (JMKF) katika kusaidia kutatua changamoto mbali mbali hapa nchini na katika Bara la Afrika. Wakazi hao waliohojiwa walisema Kikwete ni mwanadiplomasia anayekubalika kimataifa na hivyo atakuwa na uwezo mkubwa wa kuvutia rasilimali fedha kutoka kwa wafadhili katika taasisi yake. Pia walisema ingawa taasisi hiyo ni ya kimataifa wana imani Watanzania watafaidika zaidi. Musa Ali mkazi wa Temeke jijini Dar es Salaam akizungumza na gazeti hili amesema kuwa ana imani kubwa na taasisi hiyo kuwa itashughulikia vema matatizo ya binadamu siyo tu Tanzania bali Afrika nzima. “Nina imani kubwa sana taasisi hiyo itawezesha kusaidia kutatua changamoto zilizobainishwa kama za afya, elimu na kadhalika,” alisema John Barnaba wa Mbeya. Naye, Khadija Hija wa Kimara alisema kuwa ana imani na taasisi hiyo kuwa italeta matumaini makubwa nchini na kusaidia katika suala zima la maendeleo. “Kwanza mimi nina imani kubwa na Rais wetu mstaafu Jakaya Kikwete, hivyo kupitia taasisi yake hii sina shaka kabisa kuwa itasaidia mno katika suala zima la maendeleo endelevu,” alisema Bi Hija. Jumatatu wiki hii, Rais huyo Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alizindua bodi ya taasisi yake na kueleza kuwa taasisi hiyo itajikita katika kushughulikia mambo makuu manne ambayo ni maendeleo endelevu, elimu, afya na utawala bora. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo Dar es Salaam, Rais huyo mstaafu alisema wamechagua hayo mambo manne baada ya kutafakari kwa kina huku akisema lengo la taasisi hiyo si kushindana na mtu. “L engo la taasisi hii si kushindana na mtu, bali tutashirikiana na taasisi nyingine, serikali na wadau mbalimbali ndani ya nchi, barani Afrika na duniani kote kuhakikisha tunatimiza shabaha ya taasisi,” alisema Kikwete. Wajumbe wa bodi hiyo ni pamoja na Balozi Ombeni Sefue aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi kwa miaka minne, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, Balozi Mwanaidi Maajar ambaye kitaaluma ni mwanasheria na Profesa William Mahalu ambaye ni daktari bingwa wa upasuaji Hospitali ya Bugando, Mwanza. Wengine ni Abubakar Bakhresa ambaye ni mfanyabiashara na Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Makampuni ya Said Salim Bakhresa, Genevieva Sangudi ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kibiashara ya kimataifa ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mwendeshaji na Mkuu wa Kanda wa Kampuni ya Carlyle Group ya Afrika Kusini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*