Updates

Fuata Qur’an na Sunna upate Utukufu Kwa Allah

Qur’an ni kitabu cha Allah alichokiteremsha kwa wanadamu wa zama za mwisho kupitia Mtume Muhammad (rehema na amani ya Allah zimfikie). Pamoja na umuhimu wake, tulio wengi tumeshindwa kuitambua Qur’an nuru na muongozo wenye kudhamini mahitaji yetu. Haifai kwa Muislamu kuipuuza Qur’ an kwa namna yoyote. Allah Mtukufu anaonya: “Na mwenye kupuuza mawaidha yangu haya (Qur’an); basi atapata maisha yenye dhiki, na siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa ni kipofu, aseme: “Ewe Mola wangu! Mbona umenifufua kipofu, na hali nilikuwa nikiona?” Allah atasema kumuambia: “Ndiyo hivyo hivyo, zilikuja Aya zetu ukazisahau, (ukazipuuza) na kadhalika leo utasahauliwa (utapuuzwa). Na hivi ndivyo tutakavyomlipa kila anayepindukia mipaka, na asiyeamini aya za Mola wake; na bila shaka adhabu ya akhera ni kali zaidi na iendeleayo sana,” (Quran, 20:124-127). Hata hivyo Uislamu wa mtu haukamiliki mpaka akubali kumfuata Nabii Muhammad (rehema na amani za Allah zimshukie). Ni kwa muktadha huo, hatuna budi kuonesha mapezi yetu ya dhati kwa Mtume kupitia utekelezaji wa Sunna zake kufuatana na mfano wa wema waliotangulia (Salafi). Si hivyo tu, mafanikio ya duniani na akhera hayapatikani isipokuwa Muislamu apende au kuchukia jambo kwa ajili ya Allah, na pia kumfuata Mtume (rehema na amani ya Allah zimfikie). Licha ya Qur’an na Sunna kuwa miongozo sahihi katika maisha ya Muislamu, jambo la kusikitisha ni baadhi yetu kutilia shaka maelekezo yaliyomo ndani ya viwili hivi. Abdullah Ibn Abbas (Allah amuwie radhi) amehadithia kuwa Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) amesema: “Shikizo thabiti kabisa la imani ni kuwa na urafiki wa karibu kwa ajili ya Allah na kujitenga kwa ajili ya Allah, na kupenda kwa ajili ya Allah, na kuchukia kwa ajili ya Allah”(Twabrany). Faida za kushikamana na Sunna Kushikamana na Sunna ni jambo linaloleta mshikamano kwa kuwa huepusha faraka na uadui miongoni mwa waumini. Baadhi ya faida za kushikamana na Sunna ni hizi zifuatazo: Mosi, Sunna ndiyo njia ya kutekeleza ibada pasi na kupunguza wala kuzidisha jambo.Na kutokana na hilo, Mtume (rehema na amani ya Allah zimfikie) amesema: “Yeyote aliyefanya amali ambayo katika amali hiyo hakuna amri yetu, amali hiyo ni yenye kurudishwa (atarudishiwa mwenyewe),” (Muslim). Pili, kufuata Sunna ni sababu ya kupendwa na kuridhiwa na Allah. Mwenyezi Mungu anatuambia: “(Sema) Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume na mkienda kinyume na hivyo basi Mwenyezi Mungu hawapendi Makafiri” (Qur’an, 3:32). Tatu, Sunna ni sababu ya mtu kuepushwa na adhabu kali ya moto Siku ya Kiyama. Mwenyezi Mungu anasema: “…Basi na watahadhari wanaokwenda kinyume na amri ya Mtume, isije ikawapata wao misukosuko, au adhabu chungu iumizayo” (Qur’an, 24:63). Nne, Sunna humfanya mtu apambike na tabia njema. Undani wa kadhia hii unakuja katika wakati huu ambao kumekuwa na njama za makusudi za kuwatoa Waislamu kwenye utamaduni na asili ya dini yao. Licha ya kukabiliwa na changamoto hii, bado tunapaswa kujilazimisha kufuata Sunna ya Mtume katika uzito na wepesi wake. Zaidi, Mtume (rehema na amani ya Allah zimfikie) amesema: “Nimetumwa kukamilisha (kufundisha) tabia njema” (Ahmad). Na katika riwaya nyingine, Mtume amesema kumuambia Ummu Salama: “Ewe Ummu Salama, tabia njema imechukuwa kheri zote za dunia na akhera,” (Twabrany). Ewe Muislamu, tambua hakuna njia nzuri na bora ya maisha kuliko ile aliyofundisha Mtume pamoja na Maswahaba zake. Kumbuka Sunna ndiyo maisha yako, na kwa ajili hiyo yafaa uelekeze mapenzi yako kwa Mtume kabla ya wengine. Allah anatuhabarisha ndani ya Qur’an: “Ikiwa nyinyi mnampenda Allah basi nifuateni mimi (Muhammad), Allah atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Allah ni mwenye kufuta madhambi na mwenye kurehemu”(Qur’an, 3:31). Na katika hadithi, Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) amesema: “Hatoamini mmoja wenu (kuwa na imani ya kweli) mpaka anipende mimi (Muhammad) kuliko baba yake na watoto wake na watu wote,”(Bukhari na Muslim). Huu ni ushahidi kuwa, yeyote anayelichukia jambo katika yale aliyokuja nayo Mtume Muhammad atakuwa amekufuru kama walivyokufuru watu wa vitabu (Mayahudi na Wakristo). Tafiti zinathibitisha juu ya mifumo mbalimbali ya maisha ya kimagaharibi inavyoathiri mwenendo mzima wa dini kwa vijana wa Kiislamu hivyo kuwafanya waishi nje ya utaratibu (Sunna) wa Mtume. Ili kupata utukufu na heshima mbele ya Mwenyezi Mungu, hatuna budi kuishi kwa kumfuata Mtume kwa kauli na vitendo na kuepuka uzushi (bid’a). Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake wenye kufuata Qur’an na Sunna za Mtume.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*