Updates

Pendelea watu kheri na uwausie kumcha Allah

K upendeleana kheri ndiyo chimbuko la kupatikana amani, mshikamano, upendo, furaha, ukarimu, kusameheana na uadilifu miongoni mwa wanajamii. Kinyume chake ni watu kutakiana shari, jambo ambalo hupelekea chuki, bughudha na kuhusudiana. Hakika, mwenye kuwapendelea kheri waja wa Allah, mikono yake huwa baina ya mazuri na utukufu. Allah anasema: “Mema na maovu hayalingani. Pinga uovu kwa lilio jema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki, jamaa wa kukuonea uchungu,” (Qur’an, 41:34). Kadhalika, Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) amewahimiza Waislamu wawe wapendelee watu kheri: “Atakayekuwa anamuamini Allah na Siku ya Mwisho, basi na amkirimu mgeni wake, na mwenye kumuamini Allah na Siku ya Mwisho, basi na amkirimu jirani yake, na atakayekuwa anamuamini Allah na Siku ya Mwisho, basi na aseme kheri au anyamaze” (Ahmad). Kutokana na dalili mbili hizi, yafaa kutambua kuwa dunia ni shamba la kupandia mazao ya akhera, na bila shaka shamba hili litastawi na kutoa mazao bora kwa kupatikana hima ya kuwapendelea watu kheri na kuwalingania wamche Mola wao. Ni kwa sababu hiyo, Uislamu umehimiza Waumini kushikamana na ulinganiaji ili kupata fadhila za Mola wao. Ujumbe wa Uislamu ambao umeenea sehemu kubwa ulimwenguni unalenga kuwatoa watu kwenye giza la ujinga na kutakasa nafsi kutokana na upotovu. Allah anabainisha katika Qur’an: “Yeye (Mwenyezi Mungu) ndiye aliyempeleka Mtume kwa watu wasiojua kusoma, awasomee aya zake na awatakase, na awafunze kitabu na hekima, ijapokuwa kabla ya haya walikuwa katika upotofu wa wazi”, (62:2). Aya hii ni uthibitisho kwamba Allah anapowalingania kheri waja wake au kuwakataza shari ni kwa sababu anawatakia maisha mema, yenye furaha, upendo na amani. Dini Tukufu ya Uislamu imekokoteza na kuusia mno kusaidiana katika mambo ya kheri, hivyo yatupasa kufanyia kazi kauli ya Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) aliposema: “Watu wanaopendwa zaidi na Allah ni wale wenye manufaa kati yao, na matendo yapendezayo mbele ya Mwenyezi Mungu ni furaha unayoingiza katika moyo wa Muislamu, au kumuondolea matatizo, au kumlipia deni, au kumuondoshea njaa…” (Twabaraniy). Huu ndiyo wema anaopaswa kuwa nao kila Muislamu, na kutokana na hilo haijuzu kwa yeyote kuwatendea wema watu kwa kutegemea kupata fadhila kutoka kwao kwani kufanya hivyo ni kumshirikisha Allah. Swahaba Mahmud bin Labid (Allah amridhie) amehadithia kuwa Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) amesema: “Mwenyezi Mungu atasema wakati akiyahesabu matendo ya viumbe (kuwaambia waliofanya riyaa), ‘Nenda kwa wale uliokuwa ukiwaonesha matendo yako (duniani) uone kama utapata malipo yoyote kutoka kwao’”. (Ahmad). Ajabu ni kwamba, siku hizi watu hawasaidiani isipokuwa kwa maslahi fulani kama anavyosema msemaji: “Zamani rafiki alikuwa ni ‘hazina’, lakini leo urafiki ni kwa ‘maslahi’, zamani undugu ulikuwa ni ‘ngao’ lakini leo ni ‘uadui’”.

Amrisha familia yako kusimamisha Swala

Swala ni amri ya Allah na kila mchunga ataulizwa yeye binafsi na familia juu ya ibada ya Swala. Allah Mtukufu anatumbia ndani ya Qur’an: “Na waamrishe watu wako (ewe Muhammad) kuswali, na uendelee mwenyewe kwa hayo. Sisi hatukuombi wewe riziki, bali sisi ndiyo tunakuruzuku. Na m w i s h o m w e m a n i k w a wachamungu”(20:132). Kuiamrisha familia kuswali ndiyo ulikuwa mwenendo wa Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) pamoja na Maswahaba wake. Hivyo, kila mchunga ana wajibu wa kuokoa watu wake kwa kuwaamrisha kufanya ibada mbalimbali, ikiwemo ya Swala. Mbali na kuokolewa na adhabu ya akhera, mtu anayethibiti katika kusimamisha Swala Tano, Allah humjaalia riziki kwa njia nyepesi na rahisi. “Na anayemcha Mwenyezi Mungu humtengenezea njia ya kutokea. Na humruzuku kwa njia asiyotazamia (asiyotarajia).Na anayemtegemea Mwenyezi Mungu yeye humtosha…”(Qur’an, 65:2 -3). Pamoja na kuwajibika juu ya utafutaji riziki, pia ni muhimu kuhakikisha wanafamilia wanasimamisha Swala za faradhi na Sunna sanjari na ibada nyinginezo ikiwemo ya kujifunza na kusoma Qur’an. Ewe Muislamu fahamu kitendo cha kuwapendelea watu kheri na kuwalingania kumcha Allah kina malipo makubwa mbele ya Allah. Na kwa ajili hiyo, Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) amesema: “Mambo mengi yatakayowaingiza watu wengi peponi ni kumcha Allah na kuwa na tabia njema” (Tirmidhi na Hakim). Muhimu tuyachukue na kufanyia kazi maelekezo ya Allah na Mtume wake, na kufanya hivyo ndiyo salama yetu hapa duniani na kesho akhera.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*