Updates

Maisha Na Itikadi Ya Sheikh Muhammad Bin Abdulwahhab;

Sehemu ya 9,Utangulizi: Wiki iliyopita, tulimalizia kuelezea itikadi ya Sheikh Muhammad bin Abdulwahhab (Allah amrehemu), na kisha kuanza kuelezea ulinganiaji wake. Sasa endelea

Da’wah ya Sheikh Ibn

Abdulwahhab (mwendelezo)

Kazi ya da’wah ya Sheikh Muhammad bin Abdulwahhab (Allah amrehemu) inajieleza yenyewe na inakanusha kila aina ya uongo na uzandiki dhidi yake. Miongoni mwa kazi alizozifanya ni kukata miti ambayo Waislamu wa Najd walikuwa wakiiabudu na kuiomba kwa itikadi zao mbali mbali, maombi ambayo yalipaswa kuelekezewa Allah Ta’ala pekee. Miti aliyoikata ilifanana na ile waliyokuwa wakiabudu Waarabu zama za ujahili iliyojulikana kama “Dahaat N-nu’aat” ambayo Mtume Muhammad (rehema na amani za Allah zimshukie) aliarisha ikatwe kuwatoa watu katika shirki hiyo. Kwa kutegemea mafundisho ya Qur’an na Sunna, Sheikhul Islaam, Muhammad bin Abdulwahhab (Allah amrehemu), aliamrisha pia kuvunjwa vibanda (Adhrihah) vilivyojengwa juu ya makaburi ya watu waliodaiwa kuwa masharifu wenye makarama. Watu walidanganywa na kuyafanya makaburi hayo sehemu za kutembelea na kuabudu kwa ibada mithili ya ibada za kipaganii huku wakiamini kuwa waliolala makaburini humo wanaweza kunufaisha walio hai kwa shida zao mbalimbali. Masheikh waliopotea walikuwa wanawadanganya watawala na watu wote kwa ibada za kizushi na shirki mbalimbali. Kibaya zaidi, masheikh hao waliufarakanisha umma kwa kudai kuwa Sheikh Muhammad bin Abdulwahhab hampendi Mtume Muhammad (rehma na amani za Allah zimshukie). Walidai hivyo kwa kusingizia kuwa anawachukia watukufu (masharifu) na hivyo kupanda mbegu ya chuki dhidi ya Sheikh Muhammad bin Abdulwahhab (Allah amrehemu) na wafuasi wake wakati yeye alikuwa akipinga tu uzushi na shirki bila kujali zinafanywa na nani. Ili kuwaweka watu mbali na juhudi za ulinganiaji za Sheikh Ibn Abdulwahhab (Allah amrehemu), wapinzani wake walibuni jina na kuiita ulinganiaji wake, “Da’wat Wahaabiyyah” yaani Wahabiya au Wahabbism kwa Kiingereza. Jina hili lilitokana na na jina la baba yake Sheikh Muhammad la Abdulwahaab ambalo maana yake ni ‘Mja wa Al-Wahhaab’. Al-wahhab ni jina katika majina 99 ya Allah Ta’ala lenye maana ya ‘Mpaji’ au mwenye kuwapa vipawa viumbe. Wapinzani wake waliyajua na wanayajua yote haya kwamba “Wahhabiyyah” ni mtu mwenye kumuabudu ‘Al-Wahhaab’ ambaye ni Allah Ta’ala lakini wao walikusudia kuonesha kuwa amekuja na dini mpya ambayo si ya Ahlu Sunna wal Jamaa. Ukweli ni kwamba, Sheikh Muhammad bin Abdulwahhab (Allah amrehemu) alikuwa mfuasi wa madhehebu ya Imam Ahmad bin Hambal (Allah amrehemu), mmoja wa maimamu wakubwa wa Ahlu Sunna Wal Jamaa. (Tazama Kashfu AsShubhaat Fiy At-tawhid, kitabu cha Sheikh Muhammad bin Abdulwahhab). Walioshadidia sana jina hili na kuiita da’wah ya Sheikh Muhammad bin Abdulwahhab (Allah amrehemu) walikuwa ni watawala wa dola ya Kiislamu ya Waturuki na Waingereza kwa sababu mbalimbali. Waturuki, daima hawakuwa wakitaraji kwamba Waarabu watainuka tena na kuwa na dola na ulinganiaji wa kiwango cha Sheikh Muhammad bin Abdulwahhab (Allah amrehemu) ikiungwa mkono na mtawala wa Di’riyyah Muhammad bin Saud. Da’wah ya Sheikh Muhammad bin Abdulwahhab ilikuwa tishio kwa Waturuki. Kwa hiyo, watawala wa dola ya Uturuki yaani ‘Ottoman Empire’, wakawa maadui wakubwa wa da’wah ya Sheikh kwa kuhofia kudondoka kwa ushawishi wa utawala wao. Hata vitabu vya mwanzo mwanzo vya kuipinga da’wah yake Sheikh Muhammad bin Abdulwahhab viliandikwa na kusambazwa na Waturuki. Kwa upande wa Waingereza, wao walihofia kusimama kwa Uislamu uliojengwa katika misingi ya Qur’an na Sunna katika Mashariki ya Kati kutakuwa tishio kwao, hivyo wakahusisha idara ya ujasusi ya nchi hiyo kuipiga vita da’wah ya Sheikh Muhammad bin Abdulwahhab. Waingereza wakandaa propaganda kubwa dhidi ya da’wah ya sheikh na hata yale madai ya wapinzani wa Sheikh Muhammad bin Abdulwahhab (Allah amrehemu) kwamba hakuwa anajua dini bali alifundishwa dini na jasusi wa Kiingereza aitwaye Hamphrey ili kuubomoa Uislamu, ni propaganda ya majasusi Waingereza. Lengo la wote hao ni kuwaogofya watu ili wamchukie na hatimaye wasiizingatie da’wah ya Sheikh Muhammad bin Abdulwahhab (Allah amrehemu) kwa madai kuwa ameleta dini mpya

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*